Dira, Malengo na Umahiri wa Jumla
Mtaala wa Mafunzo ya Stashahada ya Ualimu Elimu ya Msingi umezingatia dira ya elimu, malengo makuu ya elimu nchini Tanzania, malengo ya elimu ya ualimu na umahiri unaotarajiwa kujengwa kwa mwalimu tarajali.
2.1 Dira
Kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi na mitazamo chanya anayethamini usawa, haki na elimu bila ukomo katika kuleta maendeleo endelevu ya kitaifa na kimataifa.
2.2 Malengo Makuu ya Elimu Tanzania
Malengo makuu ya elimu Tanzania ni kumwezesha kila Mtanzania:
- Kukuza na kuboresha haiba yake ili aweze kujithamini na kujiamini;
- Kuheshimu utamaduni, mila na desturi za Tanzania, tofauti za kitamaduni, utu, haki za binadamu, mitazamo na matendo jumuishi;
- Kukuza maarifa na kutumia sayansi na teknolojia, ubunifu, fikra tunduizi, uvumbuzi, ushirikiano, mawasiliano na mtazamo chanya katika maendeleo yake binafsi, na maendeleo endelevu ya taifa na dunia kwa ujumla;
- Kuelewa na kulinda tunu za taifa ambazo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uaminifu, uwajibikaji na lugha ya taifa;
- Kujenga stadi za maisha na stadi za kazi ili kuongeza ufanisi katika maisha ya kila siku;
- Kukuza tabia ya kupenda na kuheshimu kazi ili kuongeza tija na ufanisi katika uzalishaji na utoaji wa huduma;
- Kutambua na kuzingatia masuala mtambuka ambayo ni pamoja na afya na ustawi wa watu (jamii), usawa wa kijinsia, usimamizi na utunzaji endelevu wa mazingira; na
- Kukuza ushirikiano wa kitaifa na kimataifa, amani na haki kwa kuzingatia Katiba ya nchi na mikataba ya kimataifa.
2.3 Malengo ya Elimu ya Ualimu
2.3.1 Lengo Kuu la Elimu ya Ualimu
Kumwandaa mwalimu mwenye weledi na umahiri wa kuwezesha ufundishaji na ujifunzaji unaoendana na mabadiliko ya kisayansi, kiteknolojia, na kijamii ili kumjenga
Mtanzania mwenye maarifa, stadi na mitazamo chanya, anayethamini usawa, haki na elimu bila ukomo.
2.3.2 Malengo Mahususi ya Elimu ya Ualimu
Malengo mahususi ya elimu ya ualimu ni kumwezesha mwalimu tarajali:
- Kukuza uelewa wa kinadharia wa elimu ya ualimu, maadili ya kazi ya ualimu, maadili ya maisha, na misingi ya ualimu;
- Kujenga umahiri katika mbinu za kufundishia na kujifunzia;
- Kujenga umahiri katika mbinu za upimaji na tathmini kwa kuzingatia dhana ya ujenzi wa umahiri;
- Kukuza ubunifu na uvumbuzi katika ufundishaji na ujifunzaji kwa kuzingatia mahitaji ya mwanafunzi;
- Kutumia TEHAMA na teknolojia saidizi katika ufundishaji na ujifunzaji;
- Kukuza stadi za utambuzi wa awali kwa mwanafunzi mwenye mahitaji maalumu ya ujifunzaji na kutoa afua stahiki;
- Kuimarisha matumizi ya lugha katika ufundishaji na ujifunzaji;
- Kujenga stadi zinazolenga kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na upimaji (yaani, classroom-based research).
2.4 Umahiri wa Jumla wa Mafunzo ya Stashahada ya Ualimu Elimu ya Msingi
Umahiri wa Jumla wa Mafunzo ya Stashahada ya Ualimu Elimu ya Msingi unalenga kumwezesha mwalimu tarajali:
- Kutumia nadharia na misingi ya ualimu katika ufundishaji na ujifunzaji;
- Kumudu mbinu za kufundishia na kujifunzia;
- Kumudu mbinu za upimaji na tathmini kwa kuzingatia ujenzi wa umahiri;
- Kumudu mbinu za ubunifu na uvumbuzi katika ufundishaji na ujifunzaji kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi;
- Kutumia TEHAMA na teknolojia saidizi katika ufundishaji na ujifunzaji;
- Kumtambua mwanafunzi mwenye mahitaji ya ujifunzaji na kutoa afua stahiki;
- Kutumia lugha husika kwa ufasaha katika ufundishaji na ujifunzaji;
- Kutumia stadi za uongozi katika taaluma (instructional leadership); na
- Kumudu stadi zinazolenga kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na upimaji (yaani classroom-based research).
Sehemu ya Tatu
Maudhui ya Mtaala
Sehemu hii inafafanua maeneo ya ujifunzaji, masomo, umahiri mkuu na umahiri mahususi kwa Mafunzo ya Stashahada ya Ualimu Elimu ya Msingi.
There are no items in the curriculum yet.